5 Mei 2025 - 23:32
Source: Parstoday
Russia yasisitiza: Iran iko sahihi kabisa, haki za kinyuklia za kila nchi haziwezi kupingwa

Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Mashirika ya Kimataifa yenye makao yao mjini Vienna ametilia nguvu msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu haki yake ya kumiliki mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia na kusisitiza kwamba haki za kinyuklia zilizonazo nchi wanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Atomiki (NPT) haziwezi kupingwa wala kukanushwa.

Mikhail Ulyanov, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Nafadhilisha kujizuia kutoa maoni kuhusiana na masuala kwa undani katika hatua hii nyeti ya mazungumzo, lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko sahihi kabisa."

Ulyanov ameongezea kwa kusema: "Kwa mujibu wa NPT, nchi wanachama hazibebi jukumu tu la kutekeleza baadhi ya masharti, lakini pia zina haki za kimsingi ambazo haziwezi kutiliwa shaka".Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, alijibu matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye kwa mara nyingine tena alidai kwamba Iran inapasa ipigwe marufuku kurutubisha madini ya urani; na akasisitiza kwamba "kurudia madai ya uwongo hakubadilishi ukweli wa kimsingi."

Araghchi alibainisha kuwa, Iran, ikiwa ni mmoja wa watiaji saini waanzilishi wa mkataba wa NPT ina haki ya kumiliki mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia. Isitoshe, mbali na Iran, kuna wanachama kadhaa wa NPT ambao wanarutubisiha urani ilhali wanapinga pia kikamilifu silaha za nyuklia. Aidha, klabu hiyo, mbali na Jamhuri ya Kiislamu inajumuisha pia nchi kadhaa za Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini".

Araghchi ameendelea kueleza kwamba, kutangaza msimamo wa vikwazo vya juu kabisa na kuporoja kauli za uchochezi hakutakuwa na matokeo mengine yoyote zaidi ya kuharibu fursa ya kupatikana mwafaka katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametanabahisha kwa kusema, makubaliano yenye itibari na ya kudumu yanaweza kufikiwa, lakini kitu pekee kinachohitajika ni nia thabiti ya kisiasa na mtazamo wa kiinsafu.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha